Jumapili, 16 Machi 2014

ULAWITI KIBAHA WACHUKUA KASI



Baadhi ya wanafunzi wa kiume katika shule za msingi wilayani  Kibaha, Pwani, wamejiingiza katika vitendo vya kujaamiana wenyewe kwa wenyewe na watu wengine kutoka nje ya shule na kufikia hatua ya kupasua kaptula zao makusudi ili kurahisisha vitendo hivyo.
Shule hizo zipo katika mji wa Mlandizi mkoani humo na vimesababisha wanafunzi hao kuporomoka kimasomo kwa kuwa wanatumia muda mwingi kukaa machimbo ya mchanga na vichakani kwa ajili ya kufanya vitendo hivyo.
Katika uchunguzi uliofanywa na NIPASHE imebainika vitendo hivyo hufanywa nyakati za asubuhi wakati vipindi vya masomo vinaendelea na jioni mara wanapotoka shuleni.
Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, mahudhurio ya wanafunzi kwenye shule hizo yamekuwa ya kusuasua na kusababisha walimu kuwa na kazi ya ziada ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Uchunguzi huo umefanywa katika shule za msingi za Mtongani, Azimio na Jamhuri zote zipo ndani ya mji huo wa  Mlandizi.
JINSI HALI ILIVVO
Katika hali inayoonyesha kuwa ni mbaya kwenye shule hizo, baadhi ya wanafunzi wameonekana kuathirika kisaokolojia na kupungukiwa na uwezo wa kimasomo darasani.
Hata hivyo, afya za wanafunzi hao zipo hatarini kutokana na hofu ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwamo Ukimwi baada ya watu wazima kuhusishwa kuwaingilia.
Baadhi ya walimu wa shule hizo walipozungumza na gazeti hili walikiri kuwapo kwa vitendo hivyo  na kwamba vimeongezeka kwa kasi ya kutisha na kuwapa hofu.
Walisema walengwa wa vitendo hivyo ni wanafunzi kuanzia darasa la tatu hadi la nne ambao mara nyingi wanalazimishwa kulawitiwa na wanafunzi wenzao wa madarasa ya juu.
Aidha imedaiwa wanafunzi wengine wanafanyiwa vitendo hivyo na watu wazima wakiwa nyumbani kwao na kwenye mabanda ya kuonyesha picha za video nyakati za usiku.
"Tatizo  hili limekuwa kubwa, walimu tumejitahidi kupambana nalo kwa kiasi kikubwa lakini inaonyesha hatujafanikiwa," alisema Mwalimu Jamila Kipengele wa Shule ya Msingi Mtongani.
Mwalimu Kipengele ambaye anaongoza kitengo cha taaluma, alisema vitendo hivyo vinafanyika katika maeneo hayo ambapo huko wanafunzi wanakutana mara wanapofanikiwa kutoroka wakati wa vipindi vya masomo.
"Tunavyosikia huko machimbo wanakuwa watoto kutoka shule tofauti na kutendeana matendo hayo machafu, baada ya kugundua jambo hilo tuliamua kufanya msako mkali wa kuwakamata wote wanaohusika na kuwarudisha shuleni," alisema Kipengule.
Kwa shule ya Azimio, Mwalimu Emmanuel Mwambeja ambaye anafundisha darasa la tatu, alieleza nusu ya wanafunzi 98 wa darasa lake hawaingii darasani katika vipindi vya jioni na badala yake wanaishia kwenye machimbo.
Mwalimu Tetula Kessy wa Shule ya Msingi Azimio, ambaye yupo kwenye kamati ya kuzuia unyanyasaji wa watoto chini ya Plan Tanzania, alisema wanafunzi wengi wanajikuta wakiingia katika vitendo hivyo kutokana na kushawishiwa na watu wazima na kuangalia picha za ngono kwenye mabanda yaliyozunguka kila eneo kwenye shule hizo.
"Tunapokaa na kuwauliza kwa nini wanafanya hivyo, wanajibu kwamba walikuwa wakifanyiwa nyumbani au wanaona kwenye vibanda vya video na wao wanajaribu kwa wenzao," alisema Mwalimu Kessy.
WATOTO WASEMA
Katika Shule ya Msingi Jamhuri baadhi wanafunzi wameeleza upo wakati wanafunzi walifikia hatua ya kupasua kaptula zao upande wa nyuma ili kurahisisha kuingiliwa na wenzao.
Baadhi ya wanafunzi ambao majina yao yanahifadhiwa, walisema wanafunzi hao walikuwa na kawaida kwenda kwenye korongo lililo jirani na shule hiyo na kisha kulawitiana.
"Wanachana kaptula sehemu ya nyuma kwa kutumia wembe, tulikuja kugundua wanaporudi darasani wanakuwa katika hali tofauti ndipo tukaamua kuripoti kwa walimu," alisema mwanafunzi mmoja.
Kauli za wanafunzi hao ziliungwa mkono na Mratibu wa Elimu Kata ya Kilangalanga, Thomas Tito, ambaye alisema amefanya juhudi kubwa kupambana nalo wakati alipokuwa Mwalimu Mkuu katika shule hiyo.
"Nakumbuka nilipokuwa naongoza shule hiyo niliwakuta wanafunzi wamepasua kaptula zao kwa nyuma na wembe, nilipodadisi niligundua wanafanya mchezo huo hatari kwa sababu wanapotoka huko vichakani wanakuwa wamechafuka sana," alisema.
Kufuatia hali hiyo aliamua kuripoti katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua lakini ilishindikana baada ya kuonekana watoto hao walikuwa wakilawitiana wenyewe kwa wenyewe.
"Polisi walishindwa kuendelea kufuatilia na kuachia jukumu hilo uongozi wa shule, nilichofanya niliwaita wazazi kuwaeleza jambo hilo pamoja na kuwachukulia hatua ya kinidhmu wahusika," alisema mwalimu Tito

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni